MADHARA yatokanayo na dawa za ARVs kwa baadhi ya watumiaji hapa nchini yanahitaji ufumbuzi wa haraka ili kuweza kuondokana na tatizo hilo.


Hivi karibuni, vyombo vya habari vimeripoti tukio la kusikitisha lilitokea mkoa wa Mtwara kwamba kuna mwanaume anayeishi na virusi vya UKIMWI amebadilika maumbile yake na kuota matiti kama mwanamke katika kifua chake baada ya kuanza kutumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV). 


Alipotoa taarifa kwa daktari aliambiwa hali hiyo ni ya kawaida kwa watu ambao wanatumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo kwa muda mrefu.


Sikika imeguswa na matukio yanayotokana na utumiaji wa dawa hizo na kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi. Pamoja na baadhi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU), kutoa taarifa ya kuwa dawa wanazotumia zinawaletea madhara makubwa, bado baadhi wa watoa huduma husika wamekuwa hawachukui hatua yoyote juu ya ubadilishaji wa dawa hizo kwa WAVIU.


Kutokana na taarifa kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa dawa hizo wamepatwa na madhara mengi ambayo ni uzito kupungua, mwili kuchoka, miguu na mikono kufa ganzi, mapele, kucha kubadilika rangi kuwa nyeusi na pia baadhi yao kubadilika kimaumbile pindi tu wanapoanza kutumia dawa hizo. 


Utaratibu uliopo ni kwamba mtumia dawa hizo anapoona athari zinaanza kutokea anapaswa kutoa taarifa kwa muuguzi wake ili aweze kubadilishiwa dawa nyingine lakini imegundulika kuwa mgonjwa anapotoa taarifa juu ya madhara hayo humchukua zaidi ya miezi sita kabla ya kubadilishiwa dawa na wakati mwingine huambiwa kuwa hali hiyo ni ya kawaida na itaisha.


Sikika pia imegundua kuwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma hizo havina mashine za CD4. Kifaa hiki ni muhimu kwa ajili ya kujua maendeleo ya mgonjwa na kutoa ushauri katika kinga za mwili na pia kuendelea na aina ya dawa wanazotumia. Tatizo hili limeendelea kuwa sugu hasa katika maeneno ya vijijini ambapo WAVIU wanalazimika kwenda mwendo mrefu sana kwa ajili ya vipimo vya hivyo. Suala hili limeonekana wazi katika wilaya za Kondoa na Mpwapwa ambapo baadhi ya vituo vya afya havina mashine za CD4. 


Vituo hivyo ni Kisese, Hamai, Songolo, Busi na Kwa Mtoro vinavyopatikana wilayani Kondoa na vituo vya afya vya Kibakwe, Rudi, Mima na Pwaga vilivyopo wilaya ya Mpwapwa.Ukosekanaji wa kifaa hiki kwa kiasi kikubwa unachangia mgonjwa kuendelea kutumia aina ya dawa moja ambayo huenda haimfai tena kulingana na CD4 zake kutojua kama zimepanda au zimeshuka.


Sikika inapendekeza kuwa hatua kali zichukuliwe kwa watoa huduma ambao hawafuati utaratibu wa maadili ya kazi zao. Wizara husika pia iwajibike katika kuwasaidia wale ambao wameathirika kutokana na madhara ya utumiaji wa dawa hizo. Mfumo wa sasa wa kusikiliza matatizo ya watumia huduma uimarishwe ili kupunguza athari kubwa zinazotokana na madhara ya kutumia madawa hayo kutokana na wahudumu wengi kutumia lugha chafu.


Pia serikali inapaswa kuweka mashine za CD4 kwenye vituo ambavyo havina na kuzifanyia matengenezo haraka pale zinapoharibika ili zitumike kuwapima wagonjwa maendeleo ya kinga zao za mwili kabla hawajaanza matumizi ya dawa hizo ili kuondokana na tatizo hilo kubwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...